Si Kuku Wala Mayai ~ Na NDONE James

MAISHA ya chuo kikuu ni kama panya, huuma na hupuliza. Muhula mpya ukianza maisha huwa yanauma yakipuliza, lakini siku zikizidi kusonga, huwa yanawasha kama upupu. Wa kupuliza hayupo. Naam, baada ya kula kuku, wala mayai na muhula ukielekea kuisha wala kama kuku. Huu ndiyo mtafaruku wa maisha. Ndiko kuhangaika ili unyoroshe maisha yako ya usoni.
Nimekuwa nikifuatilia kwa makini maisha ya wanafunzi wengi hapa chuoni. Ungetembelea duka letu la chipsi mwanzo wa muhula, hungepata kuku baada ya saa moja unusu jioni. Naam, mapeni yalikuwa maridhawa, mpaka kuku walikuwa wakilalamikia Jalali, “mbona twafa hivi Baba Yetu? Hawa ndugu zetu wenye miguu mirefu kutuliko wanatumaliza.” Naye Mungu wa maskini halali, akaanza kufanya mifuko iwe miepesi. Mabadiliko yanatokea ghafla, si kuku tena, zamu ya mayai inabisha hodi.
Wakati mayai yanashika hatamu, wanafunzi hupiga moyo konde na kusema, yai ndiyo mzazi wa kuku. Je, ni binadamu yupi atalinganisha kuku na yai? Eti petroli ya kuku ni yai! Jamani hata zuzu hawezi kumanya mbinu ya ulinganisho huo duni .
Mayai huliwa kwa muda na bila shaka gurudumu la maisha linazidi kusukumwa, kwani hauko chuoni kuishi miaka na mikaka. Lakini athari za kula mayai ni nyingi. Mojawapo inabainika vizuri na wapenzi wa muziki wa aina ya Bongo, pale mwimbaji gwiji kutoka Tanga almaarufu Ali Kiba kwenye kibao chake cha Usiniseme baada ya kula mayai ‘kilichofuata watu hawakukaa.’
Soko la mayai hufungwa muhula ukikaribia tamati. Wanafunzi huwa hawana budi ila kula kama kuku. Hebu piga picha jinsi kuku huchokora taka pipani ili awaambulie riziki wanawe, haswa mkate wa kila siku.
Hayo ndiyo maisha ya mwanafunzi wa chuo kikuu wakati jua la muhula linakaribia kutua. Anarejea maisha ya kozi ya kila mtu, almaarufu common course; sukumawiki. Ukitazama wengi waliokuwa wameota vitambi utaduwaa kuona jinsi matumbo yao yalivyopigwa randa. Utadhani dau lao la maisha linakaribia ukingoni.
Hata hivyo,maisha huwa na nyakati ama pia misimu tofauti. Wakati wa kutabasamu na kulia. Msimu wa furaha na majonzi. Wakati wa kupata na kukosa. Kwa hivyo tunapaswa kukaa ange na tuyakubali maisha jinsi yanavyotupata. Usidhani kukosa ni laana, bali ni wingu linalopita tu.
Kadhalika, hauko chuo kikuu kudumu. Hapa ni ukumbini. Upo tu kwa muda, utimize majukumu yako na baadaye uende upambane na dunia. Tafakari hayo.

Mwandishi ni Mwanafunzi wa mwaka wa tatu, Mawasiliano na Uanahabari

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s