Kenya Yachomeka! ~ Na James NDONE

Mungu ni mzazi. Bila shaka ukimkosea mvyele wako hugaghibika. Naam , huenda akalipuka kwa hasira. Adhabu yake itawaandama waja wake. Lakini Mola huwa haadhibu watu kwa kiwango hiki, haswa nchi yetu ya Kenya na masaibu anuwai yanayotusibu. Si Wakenya kufa kwa sababu ya janga la njaa, si Wakenya kuangamia kwa mikasa ya moto, na si mauti ya ajali nyingi za barabara.Twaelekea wapi? Kwani tumemwasi Baba Yetu?
Wakenya bado wamegubikwa na lindi la simanzi kufuatia ajali ya moto uliosababishwa na kulipuka kwa bomba la mafuta katika kitongoji duni cha Sinai. Takriban Wakenya mia moja waliangamia. Swali kuu ni, je ni Mungu anatuadhibu kwa mawi tuliyoyatenda, ama ni Wakenya kujitia hamnazo tu na kupuuza majukumu?
Kama tujuavyo, mzizi wa vifo vya Sinai ni mafuta. Tukiangalia kumbukumbu zetu tunapata jinsi Wakenya walivyoangamia mnamo mwaka wa 2009, Februari, pale Wakenya walivyokimbilia mafuta eneo la Sachangwan, Salgaa, kilomita chache kutoka mji wa Nakuru. Haya yalitokea siku chache tu baada ya mkasa wa moto wa Nakumatt. Moto!
Miaka mitatu baadaye eneo la Sinai lapata pigo kubwa pale wenyeji wake walikumbana na mauti. Chanzo cha mkasa huu ni moto pia. Mbona tusielimike na kujua sisi ni vyumba vya udongo na hatuwezi kuhimili vishindo?
Huku bado biwi la simanzi likizidi kutanda, Wakenya wengine waliangamia eneo la Busia hapo juzi wakichota mafuta. Vya bwerere ni vya bei ghali, ni msemo usio na maana kwa mahuluki wa Kenya. Tutaelimika lini jamani?
Tukiacha hayo, tunaangazia ajali nyingi za barabarani. Kila siku kwenye vituo vya redio, runinga na pia wavuti utasikia au kusoma jinsi tunavyopoteza maisha ya Wakenya wengi. Eneo la Manyani kwenye barabara kuu ya Nairobi- Mombasa ndilo la hivi karibuni kuhusishwa na ajali mbaya. Inaonekana kuna mtu anayesinzia kazini na kama hatua mwafaka hazitachukuliwa huenda tukapoteza watu wengi. Ni vigumu kujua ni madereva ambao hawajamakinika au ni Wizara ya Uchukuzi isiyojali masilahi ya Wakenya wanaosafiri.
Suala la mwisho ambalo ningependa kuangazia ni jinsi shilingi ya Kenya inavyodidimia ikilinganishwa na Dola ya Marekani. Miezi mitano iliyopita Dola moja ingebadilishwa kwa shilingi 78 Kenya. Hapo jana Dola moja ilikuwa inabadilishwa kwa shilingi 99.9. Hapa kuna moto ambao unahitaji kuzimwa kabla haujateketeza nchi yetu.
Nawasihi Wakenya wenzangu wamakinike katika mambo yote wanayoyatenda ili tusiyafanye maisha yetu yawe Jehanamu. Aidha washika dau wa masuala ya fedha na uchukuzi wanahitajika kukaza kamba, kwani tukiendelea hivi tutazidi kupoteza ndugu, jamaa na marafiki wetu kwenye mikasa na ajali zinazoweza kuzuiliwa.

Mwandishi ni mwanafunzi wa Mwaka wa Tatu, Mawasiliano na Uanahabari

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s